Nini Maana ya Uislamu?
Uislamu ni: Amani, Unyenyekevu, na Utiifu.
Na kwa maana pana ni: Kujisalimisha kwa Mwenyezi Mungu kwa kumpwekesha, na kunyenyekea kwake kwa utiifu, na kujiweka mbali na ushirikina, amesema Mwenyezi Mungu: "Sivyo hivyo! Yeyote anayeelekeza uso wake kwa Mwenyezi Mungu, naye ni mtenda mema, basi ana malipo yake kwa Mola wake Mlezi; wala haitakuwa hofu juu yao wala hawatahuzunika". [Al Baqara: 112] Na amesema Mtume ï·º: "Uislamu ni kushuhudia ya kwamba hapana mola apasaye kuabudiwa kwa haki isipokuwa Mwenyezi Mungu Mmoja na kwamba Muhammad ni Mjumbe wa Mwenyezi Mungu, na kudumisha Swala na kutoa Zaka, na kufunga mwezi mtukufu wa Ramadhani, na kwenda kuhiji Makka kwa mwenye uwezo" [Ameipokea Imamu Muslim]
Nini maana ya Imani?
Imani: Ni kuitakidi kwa moyo, na kutamka kwa ulimi, na kutenda kwa viungo na kiwiliwili, amesema Mwenyezi Mungu Mtukufu: "Mabedui walisema: Tumeamini. Sema: Hamjaamini, lakini semeni: Tumesilimu. Kwani Imani haijaingia katika nyoyo zenu" [Al Hujrati: 14]. Na amesema Mtumeï·º: "Imani: Ni kumuamini Mwenyezi Mungu, na Malaika wake, na vitabu vyake, na Mitume wake, na siku ya mwisho, na kuamini Kadari kheri yake na shari yake." [Ameipokea Imamu Muslim] Na amesema Al-Hassan Al-Basri: "Imani si kwa kutamani tu, wala kwa kujipamba, lakini ni kile kilichokita ndani ya moyo, na kikasadikishwa na matendo".
Ni nani mola mlezi?
Mola Mlezi ni Mwenyezi Mungu aliyeumba na akawalea viumbe wote kwa neema zake, na ndiye muabudiwa wetu, hatuna muabudiwa zaidi yake, amesema Mwenyezi Mungu Mtukufu: "Kila sifa njema zinamstahiki Mwenyezi Mungu Mola Mlezi wa walimwengu". [Al-fatiha: 2]
Dini ni Nini?
Baadhi ya waliojazwa fikra potofu husema kuwa dini ni mfumo uliotengenezwa na binadamu kwa lengo la kumtawala binadam mwenzake, au wengine husema, Dini: Ni kitu kinachopunguza maumivu ya akili tu.
Ukweli nikuwa: Dini ni neno linalokusanya kunyenyekea na kujishusha, na humaanisha pia ibada na utiifu.
Hivyo dini ni mfumo wa maisha aliouweka Mwenyezi Mungu ili kuyaboresha maisha ya mwanadamu, na hakuwaacha waishi kama wanyama mwenye nguvu anamla dhaifu, na ili wajue ni nani aliyewaumba na akawalea, na walikuwa wapi kabla ya uhai wao, na watakuwa mazingira gani baada ya uhai wao, jambo ambalo hakuna awezaye kutoa jibu la uhakika wa maswali hayo, ila yule wa tangu na tangu muumba wa mbingu na ardhi.
Na lau tukisema kila mtu afuate akili yake inavyotaka, bila shaka, dunia ingejaa vurugu na machafuko, kwa sababu kwa kawaida akili zote haziwezi kukubaliana katika mambo yote, akili ya huyu itapingana na akili ya yule katika jambo na ya yule kadhalika, sasa je ili kuleta utulivu, amani na masikilizano tungesikiliza akili ya nani?
Dini leo zimekuwa nyingi, na watu wote wanadai kuwa wako katika njia sahihi anayoitaka Mwenyezi Mungu.
Swali la msingi la kujiuliza, ikiwa tutakubaliana kuwa dini ni mfumo aliouweka Mwenyezi Mungu, je, dini yako una uhakika wa maandiko kutoka katika vitabu vitakatifu yanayothibitisha kuwa dini yako ndio dini ya kweli?
Bila shaka dini ya Uislamu, ndio dini ya Mitume na Manabii wote hata kabla ya Muhammad, kwa sababu Uislamu maana yake ni unyenyekevu na utiifu, sidhani kama kuna Nabii wala Mtume hakuwa mnyenyekevu na mtiifu kwa Mola wake! Na ndio dini ya Mungu ya kweli, kwa sababu inamuelekeza mtu kumuabudu Mungu mmoja pekee aliyeumba mbingu na ardhi, asiye na baba wala mwana, na inamkataza mwanadamu kumuabudu mwanadamu mwenzake hata kama atakuwa na cheo kikubwa mbele ya Mwenyezi Mungu, kwani hiyo ni haki ya Mwenyezi Mungu pekee hapaswi kuelekezewa asiyekuwa yeye. Amesema Mwenyezi Mungu Mtukufu: "Bila ya shaka, Dini (ya kweli) mbele ya Mwenyezi Mungu ni Uislamu." [Al-Imran: 19]
Ni nani Nabii wa Umma huu?
Mwenyezi Mungu Mtukufu alituma katika kila taifa Mtume na Nabii kwa watu wao, kama alivyomtuma Mussa, Issa (Yesu) kwa wana wa Israeli, na hawa wote hawakutumwa kwa watu wa mataifa yote kama inavyoeleza Qur’ani pamoja na Bibilia, ulipofika wakati Mwenyezi Mungu alimtuma Nabii Muhammad, rehema na amani ziwe juu yake. Na jina lake: Ni Muhammad bin Abdillah bin Abdul-Muttwalib bin Hashim. Ambaye Alizaliwa Makkah, na mama yake ni Amina bint Wahb. Naye ni Nabii na Mtume aliyetumwa kwa watu wote. Amesema Mwenyezi Mungu Mtukufu: "Sema: Enyi watu! Hakika mimi ni Mtume kwenu nyinyi nyote." [Al-A'araf: 158] Yeye ndiye mwisho wa Mitume, na hakuna Nabii yeyote wala Mtume baada yake. Amesema Mwenyezi Mungu Mtukufu: "Muhammad si baba wa yeyote katika wanaume wenu, bali ni Mtume wa Mwenyezi Mungu na mwisho wa Manabii." [Al-Ahzab: 40] Alipata kuwa nabii pale maneno haya ya Mwenyezi Mungu Mtukufu yalipoteremshwa kwake: "Soma kwa jina la Mola wako Mlezi aliyeumba." [Al-'Alaq: 1] Na akawa mtume pale alipoteremshiwa maneno haya ya Mwenyezi Mungu Mtukufu: "Ewe uliyejigubika! Simama uonye!" [Al-Muddathir: 1-2]
Wahyi (Ufunuo) ulimshukia akiwa na umri wa miaka arobaini, na akahamia Madina miaka kumi na tatu baada ya kupewa utume, na akaishi huko kwa miaka kumi, na akafia mjini Madina akiwa na umri wa miaka sitini na tatu. Jambo la kwanza alilowafikishia watu Mtume, rehema na amani ziwe juu yake, ni Tauhidi, yaani kusema: 'Hakuna mungu mwenye kustahiki kuabudiwa isipokuwa Mwenyezi Mungu' Na Mola wake Mlezi alimuamrisha kumuomba Mwenyezi Mungu peke yake bila ya kumshirikisha yeyote pamoja naye katika dua zake, kama walivyokuwa wakifanya washirikina wa wakati wake. Mola wake Mlezi alimwambia: "Sema: Hakika mimi ninamuomba Mola wangu Mlezi, wala simshirikishi Yeye na yeyote." [Al-Jinn: 20] Na alisema Mtume, rehema na amani ziwe juu yake: "Dua ndiyo ibada." [Imepokelewa na At-Tirmidhi na akasema kwamba ni hadithi nzuri, sahihi]
Basi la wajibu kwa Waislamu ni kumuomba Mwenyezi Mungu peke yake, na wasimuombe mwingine yeyote, hata kama ni Mtume au mtu mwema (Walii), kwa sababu Mwenyezi Mungu peke yake ndiye Mwenye uwezo, na wengineo miongoni mwa wafu hawana uwezo wa kuwaondolea madhara. Amesema Mwenyezi Mungu Mtukufu: "Na wale wanaowaomba wasiokuwa Mwenyezi Mungu hawaumbi kitu, bali wao wameumbwa. 21. Ni wafu si walio hai, na wala hawajui watafufuliwa lini." [An-Nahl: 20-21]