top of page

damu za asili za wanawake

Muandaaji: Mwanachuoni

Sheikh Muhammad Bin Swaleh Al-Uthaimiin

Mwenyezi Mungu amsamehe yeye, wazazi wake, na Waislamu wote.

Damu zinazompata mwanamke, ni: Hedhi, Istihaadhwa (Damu ya ugonjwa), na Nifasi. Huu ni ujumbe mfupi katika yale yanayohitaji kubainishwa kuhusu damu hizi na hukumu zake. Sura ya Kwanza: Maana ya Hedhi, na hekima yake: Kisheria: Hedhi ni damu ya maumbile ambayo hutolewa na mfuko wa uzazi kupitia tupu ya mwanamke aliye vunja ungo kama sehemu ya afya, bila ya sababu, na katika siku maalumu. Hivyo ni damu ya maumbile isiyotokana na ugonjwa, jeraha, kuanguka au kuzaa. Na kwa kuwa ni damu ya maumbile, hutofautiana kulingana na hali ya mwanamke, mazingira yake na hali ya hewa; kwa hivyo wanawake hutofautiana ndani yake kwa tofauti zinazoonekana wazi. Lengo na hekima ya kuwepo kwa Hedhi: Kwa kuwa mtoto aliye tumboni mwa mama yake hawezi kupata lishe kama jinsi anavyopata yule aliye nje ya tumbo, wala haiwezekani, hata mama yake ambaye ndiye mwenye huruma kuliko wote kwake, kumfikishia chochote katika chakula; hapo ndipo Mwenyezi Mungu -Mtukufu- akaweka kwa mwanamke majimaji ya damu ambayo mtoto aliye tumboni hutumia kama lishe kwayo bila kuhitaji kula na kumeng'enya. Majimaji hayo huingia mwilini mwake kupitia kitovu, ambapo damu huenea katika mishipa yake, naye hupata lishe kwayo. Na kwa sababu hiyo, mwanamke anapobeba mimba hedhi hukatika kwake, hivyo hatokwi na damu ya hedhi ila mara chache; na vivyo hivyo wanawake wanaonyonyesha huwa wachache miongoni mwao wanaopata hedhi, hususani mwanzoni mwa kipindi cha kunyonyesha. Sura ya Pili: Muda wa Hedhi na Kipindi Chake: Sehemu ya kwanza: Umri ambao kwa kawaida hutokea Hedhi ni kati ya miaka kumi na mbili hadi miaka hamsini, na huenda mwanamke akapata Hedhi kabla ya hapo au baada yake, kulingana na hali yake, mazingira yake na hali ya hewa ya mahali alipo. Hivyo mwanamke atakapoona damu ya hedhi, atakuwa na hedhi, hata akiwa chini ya miaka tisa au juu ya miaka hamsini. Na hilo ni kwa sababu hukumu za hedhi Mwenyezi Mungu Mtukufu na Mtume wake -rehema na amani ziwe juu yake- wamezifungamanisha na kuwepo kwake; na Mwenyezi Mungu na Mtume wake -rehema na amani ziwe juu yake- hawakuweka umri maalumu. Sehemu ya pili: Muda wa hedhi, yaani kiasi cha muda wake: Amesema Ibnul-Mundhir (Mwenyezi Mungu amrehemu): Na baadhi ya wanachuoni wamesema: Hakuna kikomo kwa siku wala uchache wa kutoka damu ya hedhi wala kwa wingi wake. Na ushahidi wa kwanza: Ni kauli yake Mtukufu: "Na wanakuuliza juu ya hedhi. Waambie, huo ni uchafu. Basi jitengeni na wanawake wakati wa hedhi. Wala msiwaingilie mpaka watwaharike (wawe safi)..." [Al-Baqara: 222] Mwenyezi Mungu ameufanya ukomo wa zuio kuwa ni kutwaharika, wala hakuufanya ukomo huo kuwa ni kupita kwa siku moja na usiku mmoja, wala siku tatu, wala siku kumi na tano; hivyo jambo hili linabainisha kwamba sababu ya hukumu ni hedhi, kuwepo kwake au kukosekana kwake. Muda wowote hedhi ikiwepo basi hukumu huthibiti; na anapotwaharika kutokana nayo, hukumu zake huondoka. Ushahidi wa Pili: Ni kutoka katika Sahihi Muslim, kwamba Mtume rehema na amani ziwe juu yake alimwambia Aisha pindi alipopata hedhi na alikuwa amehirimia Umra: "Fanya kama anavyofanya hujaji isipokuwa usizunguke Nyumba (Al-Ka'aba) mpaka utwaharike." Akasema: Ilipofika siku ya Nahr (kuchinja) akatwaharika, akatekeleza Twawaf al-Ifadha." Hadi mwisho wa Hadithi. Tumeona wazi kwamba hakuna idadi ya uchache wala wingi wa siku za hedhi, na kwamba hiyo ndiyo kauli yenye nguvu; basi fahamu kwamba damu yoyote ya maumbile atakayoiona mwanamke ambayo haina sababu ya kidonda na mfano wake, hiyo ni damu ya hedhi bila kuuwekea ukomo wa muda wala umri; isipokuwa ikiwa itaendelea kumtoka mwanamke bila kukatika jumla, au ikakatika kwa muda mfupi kama siku moja au mbili katika mwezi, basi hiyo huwa ni damu ya ugonjwa. Na utakuja ufafanuzi wa damu ya ugonjwa na hukumu yake, Mwenyezi Mungu akipenda. Amesema Sheikhul-Islaam ibnu Taimiyya - Mwenyezi Mungu amrehemu-: Asili katika kila kinachotoka katika mfuko wa uzazi huwa ni hedhi, mpaka ithibiti dalili kwamba ni damu ya ugonjwa. Na akasema pia: Basi damu yoyote itakayoonekana ni hedhi, endapo haitajulikana kuwa ni damu ya mshipa au jeraha. Mwisho. Hedhi ya mjamzito: Mara nyingi sana mwanamke anapopata ujauzito hukatika damu ya hedhi, kama anavyosema Imam Ahmad: "Wanawake wengi hujua ujauzito kwa kukatika hedhi" Basi mjamzito atakapoiona damu, ikiwa ni kabla ya kujifungua kwa muda mfupi kama siku mbili au tatu, huku akiwa na uchungu wa kujifungua, basi damu hiyo ni damu ya uzazi (Nifasi), na ikiwa damu hiyo itakuwa kabla ya kujifungua kwa muda mrefu au kwa muda mfupi, isipoambatana na uchungu wa kujifungua, basi si damu ya uzazi (nifasi); lakini je, itakuwa ni hedhi ambayo zinathibiti kwake hukumu za hedhi, au ni damu iliyoharibika ambayo haipati hukumu za hedhi? Katika jambo hili kuna mitazamo tofauti miongoni mwa Wanachuoni, na yaliyo sahihi ni kwamba hiyo ni hedhi iwapo iko katika hali ya kawaida ya hedhi yake; kwa sababu asili katika damu inayompata mwanamke ni kuwa ni hedhi, iwapo hakuna sababu inayozuia kuhesabiwa kwake kuwa ni hedhi, na wala hakuna katika Kitabu na Sunna kinachozuia hedhi ya mjamzito. Huo ndio msimamo wa Maliki na Shaafiy. Na kwa msingi huu, hedhi ya mjamzito inathibiti kwake hukumu zile zile zinazothibiti kwa hedhi ya mwanamke asiyemjamzito, isipokuwa katika mambo mawili: Jambo la kwanza: Talaka. Ni haramu kumtaliki mwanamke anayelazimika kukaa eda akiwa katika hedhi ikiwa si mjamzito; na si haramu kumtaliki mjamzito. Kwa sababu talaka wakati wa hedhi kwa mwanamke asiye mjamzito ni kinyume na kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu: "...wapeni talaka katika wakati wa eda zao..." [At-Talaq: 1] Ama talaka ya mwanamke mwenye mimba akiwa katika hedhi, hilo halipingani; kwa sababu anayempa talaka mwanamke mwenye mimba basi amempa talaka kwa ajili ya eda yake, iwe yuko katika hedhi au yuko twahara; kwa sababu eda yake ni kwa ujauzito. Kwa hiyo si haramu kwake kumtaliki baada ya kujamiiana, tofauti na wengine. Jambo la pili: Hedhi ya mjamzito haimalizi muda wa eda, tofauti na hedhi ya mwanamke asiyemjamzito. Kwa sababu eda ya mjamzito haikomi ila kwa kujifungua, iwe anatokwa na damu ya hedhi au la. Kwa kauli ya Mwenyezi Mungu Mtukufu: "Na wenye mimba eda yao mpaka watakapo zaa." [Attwalaaq: 4]. Sura ya tatu: Matukio ya dharura yanayoathiri Hedhi Na matukio ya dharura yanayohusiana na hedhi yako katika aina kadhaa: Aina ya Kwanza: Kuongezeka au Kupungua; mfano wake ni kuwa mzunguko wa mwanamke ukiwa siku sita, kisha damu ya hedhi ikaendelea hadi siku saba; au mzunguko wake ukiwa siku saba, kisha atwaharike katika siku ya sita. Na aina ya pili: Kutangulia au kuchelewa; mfano: ada yake ya hedhi huwa mwishoni mwa mwezi, kisha akaona hedhi mwanzoni mwake, au ada yake huwa mwanzoni mwa mwezi, kisha akaiona mwishoni mwake. Na wanachuoni wametofautiana katika hukumu ya aina hizi mbili, na lililo sahihi ni kwamba: Mwanamke atakapoona damu basi hiyo ni hedhi, na wakati wowote akitwaharika kutokana nayo basi ametwaharika, iwe zimezidi siku zake za kawaida au zimepungua, na iwe zimetangulia au zimechelewa. Na dalili ya hilo imetangulia kutajwa katika sehemu iliyotangulia, ambapo sheria imeambatanisha hukumu za hedhi na kuwapo kwake. Huu ndio msimamo wa Madhehebu ya Kishaafiy, na ndio chaguo la Sheikhul-Islam Ibnu Taymiyyah, na ameuimarisha na kuutetea Mwandishi wa Al-Mughni, akasema: Lau ada ingelizingatiwa kwa namna iliyotajwa katika madhehebu, basi Mtume rehema na amani zimshukie angeliubainisha kwa Umma wake, na isingeli kuwa halali kwake kuchelewesha ufafanuzi wake.[1][2] Kwa sababu haifai kuchelewesha kubainisha mpaka ukaisha muda wake wakubainisha, na wake zake na wengineo miongoni mwa wanawake wanahitaji kubainishiwa hilo kila wakati, basi hakuwa wa kulipuuzia kulibainisha hilo. Wala hakuna kilichopokelewa kutoka kwa Mtume -rehema na amani ziwe juu yake- cha kutaja ada ya hedhi wala kuibainisha, isipokuwa katika hukumu ya mwanamke mwenye istihaadha tu.[3]. Mwisho wa kunukuu. Aina ya tatu: Maji maji ya njano au ya kahawia; kwa namna ambayo huonekana damu ikiwa ya njano kama maji ya vidonda, au iliyochanyika kati ya rangi ya njano na nyeusi. Basi haya yakitokea wakati wa hedhi, au yakaungana nayo kabla ya kutwaharika, yanazingatiwa kuwa ni hedhi; tunayathibitishia hukumu za hedhi. Na yakitokea baada ya kutwaharika si hedhi; kwa kauli ya Ummu Atwiya -radhi za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake-: "Tulikuwa hatuchukulii maji maji ya kahawia na njano baada ya twahara kuwa ni chochote" Imepokelewa na Abu Daudi kwa mlolongo mzuri wa wasimulizi[4], na pia ameipokea Bukhari bila ya kuzidisha (baada ya kutwaharika), lakini ametunga mlango kwa kauli yake: “Mlango wa maji maji ya njano na kahawia katika siku zisizo za hedhi”[5]. Amesema katika sherehe (ufafanuzi) wake Fat-hul-Baari: Anaashiria kwa hilo kuleta muafaka kati ya hadithi ya Aisha iliyotangulia katika kauli yake: "mpaka uone ute mweupe." Na imebainisha hadithi ya Ummu Atwiya -radhi za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake- iliyotajwa katika mlango, kwamba hilo, yaani hadithi ya mama Aisha -radhi za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake-  limechukuliwa kuwa linahusu pale mwanamke anapoona maji maji ya kahawia na njano katika siku za hedhi; ama nje ya siku hizo, basi (hukumu ni) kama alivyosema Ummu Atwiya -radhi za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake-.[6] Mwisho wa kunukuu. Na hadithi ya Aisha aliyoiashiria, ni lile alilolitaja Bukhari kwa yakini kabla ya mlango huu[7], kwamba wanawake walikuwa wakiagiza kipande cha kitambaa, yaani; kitu ambacho mwanamke hujitia ili ajue kama bado imebaki athari ya hedhi au la, ili iende kwa mama wa waumini Aisha radhi za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake; ndani yake kuna Kursuf yaani; pamba, ikiwa na rangi ya njano, alikuwa akisema: "Msifanye haraka mpaka muione alama nyeupe."[8] Na ute mweupe ni maji meupe yanayotoka katika mfuko wa uzazi wakati hedhi inapokatika. Na aina ya nne: Ni kukatika katika kwa hedhi, kwa namna kwamba mwanamke huona siku moja damu, na siku nyingine akawa yuko twahara na mfano wake, basi hizi ni hali mbili: Hali ya kwanza: Kuwa jambo hili liwe pamoja na mwanamke daima, muda wake wote; basi hiyo ni damu ya ugonjwa, na huthibiti kwa anayepatwa nayo, hukumu ya mwanamke mwenye damu ya ugonjwa. Hali ya pili: Isiwe inatokea kwa mfululizo kwa mwanamke, bali humjia baadhi ya nyakati, na anakuwa na wakati wa twahara ulio sahihi. Basi wanachuoni -Mwenyezi Mungu awarehemu- wametofautiana kuhusu ukavu huu: je, unahesabiwa kuwa twahara au unaingia chini ya hukumu za hedhi? Basi madhehebu ya Shafi'i katika kauli zake mbili iliyo sahihi zaidi ni kwamba hukumu za hedhi zinamhusu, hivyo huhesabiwa kuwa hedhi[9], na hilo ndiyo chaguo la Sheikhul-Islam Ibn Taimiyya na mwandishi wa al-Fa'iq[10], na ni madhehebu ya Abu Hanifa pia[11], na hilo ni kwa sababu maji maji meupe wanayajua wanawake hayaonekani katika hali hiyo; na kwa kuwa lau kingehesabiwa kuwa ni kutwaharika, basi yaliyo kabla yake yangekuwa hedhi moja, na yaliyo baada yake yangekuwa hedhi moja, na hakuna mwenye kauli hiyo; la sivyo, eda inayohesabiwa kwa mizunguko ya hedhi ingemalizika kwa siku tano. Na kwa kuwa lau kama lingewekwa kuwa ni twahara, lingesababisha tabu na ugumu wa kuoga na mengineyo kila baada ya siku mbili; na dhiki imeondoshwa katika Sheria hii, na sifa njema ni za Mwenyezi Mungu. Na kilicho mashuhuri katika madhehebu ya Hanbali ni kwamba: Damu ni hedhi, na usafi ni twahara, isipokuwa endapo jumla ya vyote viwili itazidi kiwango cha juu cha hedhi; basi damu inayozidi huwa ni damu ya ugonjwa (Istihadhwa).[12] Na amesema katika Al-Mughni: Inaelekea kwamba kukoma kwa damu kunapokuwa chini ya siku moja si twahara, kwa mujibu wa riwaya tuliyoitaja katika nifasi kwamba haizingatii kilicho chini ya siku moja; na hilo ndio sahihi -Mwenyezi Mungu akipenda-, kwani damu wakati mwingine hushuka na wakati mwingine hukoma. Na kuwajibisha kuoga kwa anayetwaharika saa baada ya saa ni tabu inayoondolewa; kwa kauli Yake Mtukufu: "Wala hakuweka juu yenu mambo mazito katika Dini." [Al-Hajj: 78] Akasema: Kwa msingi huu, kukatika kwa damu hakutakuwa chini ya siku moja ya twahara, isipokuwa aone kinachoashiria hilo, kama vile kukatika huko kukawa mwishoni mwa kawaida yake ya hedhi, au aone maji maji meupe.[13] Mwisho wa kunukuu. Hivyo, kauli hii ya Mwandishi wa Al-Mughni iko katikati ya kauli mbili, na Mwenyezi Mungu ndiye Mjuzi zaidi wa lililo sahihi. Aina ya tano: Ukavu wa damu kiasi kwamba mwanamke anaona unyevu tu. Hali hii ikiwa katika wakati wa hedhi au ikiambatana nayo kabla ya kutwaharika, basi ni hedhi; na ikiwa baada ya kutwaharika, si hedhi. Kwa sababu upeo wa hali yake ni kuhusishwa na maji ya njano na kahawia, na hii ndiyo hukumu yake. ​ [1] Tazama: Majmu'ul Fataawa: Juzuu ya 19, uk. 238-239. [2] Al-Umm (82/1). [3] Al-Mughni (396/1) [4] Imepokelewa na Abu Dawud: Kitabu cha Twahara, mlango kuhusu mwanamke anayeona rangi ya kahawia (al-kudrah) na ya njano (as-sufrah) baada ya twahara, nambari (307). [5] Imepokelewa na Bukhari: Kitabu cha Hedhi, mlango wa ute wa rangi ya manjano na kahawia katika siku zisizo za hedhi, nambari (326). [6] Fat-h Al-Baari", 1/426. [7] Sahihi Bukhari (1/ 71). [8] Ameitaja Bukhari kwa mu'allaq: Kitabu cha Hedhi, Mlango wa kuingia kwa hedhi na kutoka kwake, kabla ya hadithi nambari (320). [9] Al-Umm (1/ 83-84). [10] Imenukuliwa kutoka kwao katika Al-insaaf. [11] Al-Asl (19/2-20) [12] Al-Mughni (226/1) [13] Al-Mughni (257/1).

bottom of page