top of page

Maswali mbali mbali Ya Kisheria na Majibu Yake

Je, inafaa kuiuliza Akili Bandia (Ai) Maswala ya Kisheria?

Swali: Je, inaruhusiwa kurejea Aplikesheni za Akili Bandia (Ai) kwa ajili ya kuziuliza baadhi ya maswala ya kisheria, na kuchukua hukumu humo, na kuzifanyia kazi hukumu zake? Jawabu: Akili Bandia (Artificial Intelligence) kimsingi ni nyenzo inayoruhusiwa kutumiwa. Hata hivyo, haifai kuitumia kama chombo cha kuulizia fatwa, wala kutegemea majibu yake katika masuala ya kisharia. Hii ni kwa sababu haina sifa na uwezo unaohitajika kwa mtu anayetoa fatwa, kama vile kuwa na uelewa wa kina wa dini, kuifahamu hali halisi ya mambo, pamoja na masharti mengine yanayohitajika katika utoaji wa fatwa. Aidha, majibu yake huzalishwa kwa njia ya kiotomatiki kutokana na taarifa na takwimu ambazo huenda vyanzo vyake visiwe vinajulikana au vikawa na makosa. Vilevile, majibu hayo yanaweza kuwa na mielekeo ya upendeleo na yasizingatie tofauti muhimu zilizopo baina ya watu na mazingira yao. Hata hivyo, inajuzu kwa mtafiti kunufaika na Akili Bandia katika kukusanya taarifa na nyenzo za kielimu, au kupata ufahamu kuhusu hali halisi ya mambo, kwa sharti la kuhakiki usahihi wa taarifa hizo na vyanzo vyake. Ama mtu asiye na elimu ya kutosha ya kisharia (Muumini wa kawaida), hairuhusiwi kwake kufanyia kazi fatwa inayotolewa na Akili Bandia. Badala yake, anapaswa kuwauliza wanazuoni wenye elimu na wanaoaminika.

Je, Uislamu huwatazama wasiokuwa Waislamu kwa jicho la huruma na upole?

Swali: Je, Uislamu una mtazamo gani kuhusu ubinadamu? Je, unahimiza kuwapenda na kuwathamini watu wengine kwa kuzingatia utu wao kama wanadamu, bila kujali tofauti za dini au asili zao za kikabila? Jawabu: Ni wajibu kujua kwamba: Uislamu ni mfumo sahihi uliotoka kwa Mola Mlezi wa Walimwengu, usiokuwa na dosari ndani yake. Na Muislamu ni binadamu kama binadamu wengine, anaweza kupatia na kukosea kama Watu wengine. Hivyo, yanayofanywa na watu hayana uhusiano kabisa na Uislamu endapo yatakiuka misingi na mipaka aliyoiweka Mwenyezi Mungu Mtukufu. Mtazamo wa Uislamu kuhusu wanadamu umejengwa juu ya misingi ya rehema, huruma na upole. Na haiwezekani ukawa vinginevyo, kwa sababu dini ya Kiislamu ndiyo dini ya mwisho miongoni mwa dini alizozifanya Mwenyezi Mungu Mtukufu kuwa sheria, na akawaamrisha watu wote kuingia katika dini hiyo. Vilevile, Mwenyezi Mungu ndiye aliyeteremsha dini hii na kumteremshia Mtume wake Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam), ambaye ndiye mwenye huruma kubwa zaidi miongoni mwa viumbe. Ushahidi wa jambo hili unapatikana katika Kitabu cha Mwenyezi Mungu Mtukufu, pale aliposema: “Nasi hatukukutuma isipokuwa uwe ni rehema kwa walimwengu wote.” (Suratul-Anbiyaa: 107) Mambo Muhimu yaliyohimizwa katika Uislamu 1-Kuwaita Watu katika Uislamu, na kuwaokoa kutoka katika Ukafiri na Ushirikina. 2-Kuwatendea Wema Wazazi wawili, hata kama si Waislamu. Allah anasema: “Na tumemuusia Mwanadamu kwa Wazazi wake kuwatendea Wema…” [Luqman: 14-15] 3-Usia wa kuishi vizuri na Majirani hata kama si Waislamu. Allah anasema: “…Na Wazazi Wawili kuwatendea Wema...na jirani wa karibu na jirani wa mbali…” [An-Nisaai: 36] Amesema Imam Qurtubi katika tafsiri yake: Jirani wa karibu Yaani: Muislamu na Jirani wa mbali: Yaani: Myahudi au Mkristo. 4-Kutenda uadilifu unapoishi na asiyekuwa Muislamu, asiyewapiga vita Waislamu. Amesema Allah Mtukufu: “Mwenyezi Mungu hakukatazini kuwafanyia wema na uadilifu wale ambao hawakukupigeni vita, wala hawakukutoeni makwenu. Hakika Mwenyezi Mungu huwapenda wafanyao uadilifu” [Mumtahna: 8]. 5-Uharamu wa kumuua asiyekuwa Muislamu, aliyeingia mkataba wa amani, na karipio kali katika hilo. Amesema Mtume Muhammad rehema na amani ziwe juu yake: “Atakayemuua kafiri aliyeingia mkataba wa amani, basi hatonusa harufu ya Pepo...” [Sahihi Bukhari] 6-Uharamu wa kumdhulumu asiyekuwa Muislamu aliyeingia mkataba wa amani, na kumtwisha mzigo mkubwa zaidi ya uwezo wake. Na imekuja kutoka kwa Mtume Muhammadi rehema na amani ziwe juu yake amesema: “Tambueni! Yeyote atakayemdhulumu asiyekuwa Muislamu aliyeingia mkataba wa amani, au akamvunjia heshima, au akambebesha mzigo juu ya uwezo wake, au akachukua kutoka kwake chochote bila ridhaa yake, basi mimi ndiye nitakayesimama naye (katika mahakama ya) siku ya Kiyama” [Sahihi Abuu Daud] 7-Uharamu wa kumfanyia uadui na uwajibu wa kumtendea Wema. Anasema Allah Mtukufu: “…Wala kuchukiana na Watu kusikupelekeeni kutofanya uadilifu. Fanyeni uadilifu. Hivyo ndio kuwa karibu mno na uchamungu…” [Maaidah: 8]

bottom of page